萝莉视频

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)

Electroconvulsive therapy (ECT)

Below is a Swahili translation of our information resource on electroconvulsive therapy (ECT). You can also read our other Swahili translations.

Taarifa hii ni ya mtu yeyote anayefikiria iwapo anatakiwa kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), pamoja na familia zao au marafiki.

Wewe na madaktari wako mnapaswa kuhakikisha kuwa mna ufahamu kamili wakati wa kufanya uamuzi kuhusu iwapo utapewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) au la. Daktari wako atazungumza nawe kuhusu suala hili. Tunatumaini kuwa taarifa hii inaweza kukusaidia kufanya uamuzi huu kwa kutoa taarifa kuhusu:

  • tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni nini na kwa nini inatumika
  • ni nini kinachohusika katika utoaji wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)
  • faida za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)
  • hatari na athari mbaya za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) zinazoweza kutokea
  • kinachoweza kutokea ikiwa hutapata matibabu
  • kufanya maamuzi kuhusu kufanya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)
  • mahali pa kupata taarifa zaidi.

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni nini na kwa nini inatumika?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni matibabu yenye ufanisi kwa aina fulani za hali mbaya zaidi ya afya ya akili. Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kuzingatiwa wakati njia zingine za matibabu, kama vile tiba ya kisaikolojia au dawa, hazijafaulu au wakati mtu ni mgonjwa sana na anahitaji matibabu ya haraka.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) hutolewa kama mzunguko wa matibabu, kwa kawaida mara mbili kwa wiki kwa wiki 3-8. Ikiwa utapewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), itafanyika baada ya kupewa nusukaputi ya jumla. Hii ina maana kwamba utakuwa umelala wakati inafanyika.

Ukiwa umelala, ubongo wako utachochewa kwa kutumia mapigo mafupi ya umeme. Hii husababisha kifafa kinachodhibitiwa ambacho hudumu kwa chini ya dakika mbili. Pamoja na dawa ya nusukaputi, utapewa dawa ya kusaidia kupumzika kwa misuli ambayo inapunguza kiasi cha kusonga cha mwili wako wakati wa kifafa hicho kinachodhibitiwa.

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kutumika katika hali gani?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) hutumiwa sana kwa unyogovu mkali ambao haujaitikia matibabu mengine. Pia hutumiwa kutibu katatonia, hali isiyo ya kawaida ambayo mgonjwa anaweza kuacha kuzungumza, kula au kusogea. Mara kwa mara, hutumiwa kutibu watu walio katika awamu ya wazimu mkali ya ugonjwa wa wazimu au wakati watu wana dalili mchanganyiko za wazimu na msongo wa mawazo.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) haipendekezwi kwa matibabu ya matatizo ya wasiwasi au hali nyingine nyingi za akili. Kwa kipindi cha muda cha wastani, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kusaidia dalili za skizofrenia ambazo hazijapungua kwa kutumia dawa. Hata hivyo, manufaa ya muda mrefu, ambayo yanahitaji kuendelea kwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), sio wazi sana. Kwa sababu hii, haitumiki mara nyingi nchini Uingereza.

Je, ni wakati gani daktari wako anaweza kupendekeza tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa kawaida itapendekezwa ikiwa hali yako:

  • ni hatari kwa maisha na unahitaji kupata nafuu haraka ili kuokoa maisha yako
  • inakusababishia mateso makubwa sana
  • haijaitikia matibabu mengine, kama vile dawa unayochukua kutibu au kukinga ugonjwa na tiba ya kisaikolojia
  • imeitikia vyema kwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) hapo awali.

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ina ufanisi gani?

Madaktari wanaowatibu watu kutumia tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) wanaripoti kwamba watu wengi wanaonyesha hali ya kupungua kwa dalili zao. Katika mwaka 2018-2019, asilimia 68% ya watu waliokuwa wametibiwa kwa kutumia tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) walionekana kuwa "wamefanya maendeleo makubwa" au "wamefanya maendeleo makubwa sana" mwishoni mwa matibabu (mizunguko ya 1,361 kati ya jumla ya 2,004). Baadhi ya watu hao waliripotiwa kutoonyesha mabadiliko katika hali zao na kwa idadi ndogo sana ya watu (1%) iliripotiwa kuwa hali zao zilikuwa zinazidi kuzorota.

Kutibu msongo wa mawazo

Idadi kubwa ya ushahidi unaonyesha kwamba tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inafanikiwa zaidi katika kutibu visa vikali zaidi vya msongo wa mawazo kuliko matibabu yoyote ambayo imelinganishwa nayo. Hizi ni pamoja na:

  • dawa za mfadhaiko
  • kipozauongo - ambapo mtu hupewa dutu au utaratibu ambao hauna athari ya kimwili ili kupima ufanisi wa matibabu mapya
  • matibabu ya neuromodulationkama vile kichocheo cha sumaku ya fuvu (rTMS).

Hatari ya kujiua ni ndogo kwa watu waliopata tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ikilinganishwa na watu ambao hawapati tiba hiyo.

Kusalia mwenye afya

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kusaidia watu ambao ni wagonjwa sana kupata nafuu vya kutosha ili kupata aina nyingine za matibabu. Hii inaweza kuwasaidia kusalia wenye afya kwa muda mrefu.

Utafiti unapendekeza kwamba watu ambao wana unyogovu mkali ambao hawajapata nafuu baada ya kutumia dawa wana uwezekano mkubwa wa kupata nafuu na kubakia wenye afya kwa muda mrefu ikiwa watapata tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Kati ya watu wanaopata nafuu baada ya kupata tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), nusu yao watasalia na afya nzuri angalau kwa mwaka mmoja. Hii inawezekana zaidi ikiwa watapewa matibabu baada ya kumaliza tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), kama vile dawa ya mfadhaiko au lithiamu.

Kwa kulinganisha, watu walio na unyogovu mkali ambao hawajapata nafuu baada ya kujaribu dawa mbili tofauti za mfadhaiko wana nafasi ya 5% tu ya kupata nafuu na kubakia na afya nzuri kwa angalau mwaka mmoja ikiwa watapewa dawa ya mfadhaiko ya tatu.

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inafanyaje kazi?

Athari za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) huongezeka polepole kwa kila matibabu. Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) husababisha kutolewa kwa kemikali fulani za ubongo, ambazo zinaonekana kuchochea ukuaji wa baadhi ya maeneo katika ubongo ambayo hupungua kwa sababu ya msongo wa mawazo.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) pia inaonekana kubadilisha jinsi sehemu za ubongo zinazohusika na hisia zinavyoingiliana. Kuna utafiti unaoendelea katika eneo hili ili kutusaidia kuelewa zaidi kuhusu jinsi tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inavyofanya kazi.

Je, kuna aina tofauti za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) imebadilika na kuendelea kadri miaka inavyosonga. Kwa mfano, kiasi na aina ya umeme iliyotumiwa imebadilika. Hii imepunguza uwezekano wa kutokea kwa athari mbaya.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inatolewa kwa njia mbili: tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya pande mbili na tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya upande mmoja. Daktari wako ataweza kukueleza zaidi na kukupa ushauri kuhusu ni aina gani ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inayoweza kukufaa zaidi.

Kwenye tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya pande mbili, mipigo ya umeme hupita kwenye kichwa chako, kati ya panja zako. Kwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya upande mmoja, hupita kati ya panja lako la kulia na sehemu ya juu ya kichwa chako. Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya pande mbili inaweza kufanya kazi kwa haraka zaidi, ilhali tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya upande mmoja ina athari kidogo kwenye kumbukumbu. Kuna habari zaidi kuhusu athari mbaya baadaye katika nyenzo hii.

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kutumika kwa watoto au vijana?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) haitumiwi kwa watoto chini ya umri wa miaka 11. Watoto wenye umri kati ya miaka 11 na 18 mara chache hupata aina za magonjwa ya akili yanayoitikia vyema kwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), lakini kwa wachache wanaopata, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kusaidia. Maoni rasmi ya pili na huru yanahitajika kabla ya kutolewa kwake.

Je, ni nini kinatokea unapopokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) hutolewa hospitalini na kwa kawaida hufanyika katika seti ya vyumba vinavyoitwa 'ECT suite'. Wakati mwingine, ikiwa vyumba hivi havipo au una matatizo makubwa ya hali ya afya ya kimwili, matibabu yanaweza kufanyika katika hospitali nyingine iliyo na msaada zaidi wa matibabu, au katika chumba cha upasuaji.

Baadhi ya watu wanaopokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni wagonjwa wa kulazwa hospitalini, wakati wengine wakipokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kama wagonjwa wanaotibiwa na kurudi nyumbani. Ikiwa wewe ni mgonjwa wa anayetibiwa na kurudi nyumbani, mtu mzima aliyetajwa, anayewajibika atalazimika kuandamana nawe kwenda na kutoka kwa chumba cha tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Chumba cha tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kinapaswa kuwa na chumba cha kusubiri, chumba cha matibabu, na chumba cha kupata afueni vizuri kabla ya kuondoka.

Wafanyakazi waliohitimu watakutunza wakati wote utakuwa hapo. Wanaweza kukusaidia kujibu maswali au wasiwasi wowote ambao unaweza kuwa nao kabla ya kupata matibabu. Pia watakusaidia na mchakato wa kuamka kutoka kwa usingizi wa nusukaputi na muda mfupi mara baada ya matibabu.

Kujiandaa kwa ajili ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)

Katika siku chache kabla ya mzunguko wako wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kuanza, daktari wako atapanga baadhi ya vipimo ili kuhakikisha kuwa ni salama kwako kupata nusukaputi ya jumla. Hizi zinaweza kujumuisha rekodi ya mapigo ya moyo wako (ECG) na vipimo vya damu.

Hupaswi kula au kunywa chochote kwa angalau saa 6 kabla ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), ingawa unaweza kuruhusiwa kunywa funda chache za maji hadi saa 2 kabla. Hii ni kuhakikisha kuwa nusukaputi inatolewa kwa usalama.

Ikiwa kwa kawaida unatumia dawa wakati huu, uliza timu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa ushauri ikiwa bado unapaswa kufanya hivyo.

Je, ni nini hutokea siku ya matibabu yako ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)?

  • Ikiwa wewe ni mgonjwa wa kulazwa, mfanyakazi atakuwa nawe kwenye chumba cha ECT. Watajua kuhusu ugonjwa wako na wanaweza kueleza kinachoendelea. Vyumba vingi vya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) vinaruhusu wanafamilia kukaa kwenye chumba cha kusubiri wakati unapatiwa matibabu.
  • Utakutana na mfanyakazi wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), ambaye atafanya ukaguzi wa kawaida wa mwili (ikiwa bado haujafanyiwa).
  • Utaulizwa kabla ya kila matibabu kuhusu kumbukumbu yako na jinsi ilivyo nzuri.
  • Ikiwa unapata tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa hiari wafanyakazi wataangalia kuwa bado uko tayari kufanya, na watauliza ikiwa una maswali zaidi.
  • Unapokuwa tayari, wafanyakazi wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) watakupeleka kwenye eneo la matibabu.
  • Wafanyakazi wataunganisha vifaa vya ufuatiliaji ili kupima kiwango cha moyo wako, shinikizo la damu, viwango vya oksijeni na mawimbi ya ubongo.
  • Utapewa oksijeni kupumua kupitia barakoa. Daktari wa nusukaputi atakupa nusukaputi kupitia sindano nyuma ya mkono wako.

Je, ni nini kinatokea wakati umelala?

  • Ukiwa umelala, daktari wa nusu kaputi atakupa dawa ya kusaidia kupumzika kwa misuli na kinga ya kinywa itawekwa kinywani mwako ili kulinda meno yako.
  • Diski mbili za chuma zitawekwa kwenye kichwa chako. Katika tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya pande mbili, moja huwekwa kila upande wa kichwa chako, wakati katika tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya upande mmoja zote zinawekwa upande mmoja wa kichwa chako.
  • Mashine ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) itatoa mfululizo wa mapigo mafupi ya umeme, kwa sekunde tatu hadi nane. Hii itasababisha kifafa kinachodhibitiwa ambacho hudumu kwa wastani wa sekunde 40, na kinaweza kudumu hadi sekunde 120. Mwili wako utakuwa mgumu na kisha kutakuwa na kutetemeka, kawaida huonekana mikononi mwako, miguuni na usoni. Dawa ya kusaidia kupumzika kwa misuli hupunguza kiasi ambacho mwili wako unasonga.
  • Dozi ya mapigo ya umeme inayotolewa inategemea na kiasi kinachohitajika ili kusababisha kifafa kinachodhibitiwa. Mwitikio wako utafuatiliwa, na dozi itarekebishwa kama inavyohitajika.

Je, ni nini kinatokea unapoamka?

  • Dawa ya kusaidia kupumzika kwa misuli itaisha ndani ya dakika chache. Unapoanza kuamka, wafanyakazi watakupeleka hadi eneo la kupata nafuu. Hapa, muuguzi mwenye uzoefu atakutunza hadi utakapoamka kabisa.
  • Muuguzi atapima shinikizo lako la damu na kukuuliza maswali rahisi ili kukagua uko macho kiasi gani. Kutakuwa na kifuatiliaji kidogo kwenye kidole chako ili kupima kiwango cha oksijeni katika damu yako. Unaweza kuamka ukiwa na barakoa ya oksijeni. Inaweza kuchukua muda kuamka kabisa, na mwanzoni unaweza usijue mahali ulipo. Baada ya kama nusu saa, athari hizi zinapaswa kuisha na utaulizwa maswali machache kuthibitisha hilo.
  • Vyumba vingi vinavyotumika katika tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) vina eneo la pili ambapo unaweza kukaa na kunywa chai au kinywaji kingine chepesi. Utaondoka kwenye chumba cha tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) wakati hali yako ya mwili itakapokuwa thabiti, na utakapojihisi uko tayari kufanya hivyo.
  • Mchakato wote kwa kawaida huchukua takribani saa moja.

Ndani ya saa 24 baada ya kila matibabu, hupaswi kunywa pombe au kutia sahihi hati yoyote ya kisheria.

Unapaswa kuwa na mtu mzima anayekuwajibikia kwa saa 24.

Je, ni mara ngapi na kwa idadi gani tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inatolewa?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa kawaida hutolewa mara mbili kwa wiki, na siku chache kati ya kila matibabu. Inaweza kuchukua vipindi kadhaa kabla ya kuona mabadiliko mazuri.

Haiwezekani kutabiri, mapema, idadi ya matibabu utakayohitaji. Kwa wastani, utapokea idadi ya matibabu kati ya 9 au 10 katika mzunguko mmoja, ingawa ni jambo la kawaida kuwa na zaidi ya hayo.

Ikiwa hutapata mabadiliko yoyote baada ya matibabu ya 6, mpango wako wa matibabu utakaguliwa tena na daktari wako ili kujadili iwapo utaendelea au kubadilisha aina ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Timu yako ya matibabu itakagua maendeleo yako na athari mbaya, kwa kawaida kila wiki. Utaulizwa kuhusu kumbukumbu zako na zitapimwa mara kwa mara.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa kawaida itasitishwa muda mfupi baada ya kupona kabisa, au ikiwa utasema hutaki kuendelea nayo tena na unaelewa vya kutosha uamuzi huu.

Je, ni nini hutokea baada ya mzunguko wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)?

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni sehemu moja ya kupata afueni. Inapaswa pia kukusaidia kuanza au kuanzisha upya matibabu mengine au aina nyingine za msaada.

Kwa kawaida utaendelea au kuanza matibabu ya dawa baada ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hii itasaidia kudumisha nafuu ambayo umepata kutokana na matibabu yako ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) wakati mwingine inaweza kuendelezwa ili kukusaidia kuzuia kuugua tena. Hii hasa hutokea kwa wale ambao hapo awali waliugua tena baada ya mzunguko wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hii inajulikana kama 'kuendeleza' au 'kudumisha' tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), na hufanywa mara chache, kwa mfano kila baada ya wiki 2-4.

Tiba ya kuzungumza kama vile tiba ya tabia ya utambuzi (CBT) na ushauri nasaha zinaweza kukusaidia kuelewa sababu zozote za kuwa mgonjwa na kukuza njia za kusalia mzima mwenye afya. Mabadiliko katika mtindo wako wa maisha ya kila siku pia yanaweza kusaidia. Haya ni pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara, kula vyakula vyenye lishe, kuwa na ratiba ya kawaida ya kulala, na kutumia mbinu kama vile uangalifu na kutafakari.

Kliniki ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) au daktari wa akili aliyepanga matibabu atawasiliana nawe ili kukuuliza kuhusu kumbukumbu yako miezi 2 baada ya matibabu yako ya mwisho. Ikiwa unakumbana na matatizo ya kumbukumbu unaweza kuomba upelekwe kwa mtaalamu wa saikolojia ya neva au huduma ya tathmini ya kumbukumbu kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Je, athari mbaya za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni zipi?

Kama ilivyo kwa matibabu yoyote, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kuwa na athari mbaya.

Athari mbaya kwa kawaida huwa kidogo na ya muda mfupi lakini wakati mwingine inaweza kuwa mbaya sana na inayoweza kudumu kwa kipindi cha muda mrefu.

Hatari ya athari mbaya huongezeka kidogo ikiwa dozi za kiwango kikubwa za kuchochea mapigo zinahitajika, ikiwa wewe ni mwanamke, au ikiwa wewe ni mzee.

Ikiwa utapata athari mbaya wakati wa mzunguko wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), matibabu hayo yanaweza kurekebishwa.

Athari mbaya za muda mfupi

Mara tu baada ya kupokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), unaweza kupata:

  • maumivu ya kichwa
  • maumivu ya misuli na/au taya
  • uchovu wakati athari za nusukaputi zinapokwisha
  • kuchanganyikiwa, hasa ikiwa wewe ni mzee (hii kawaida hutoweka baada ya dakika 30)
  • ugonjwa au kichefuchefu.

Muuguzi atakuwa pamoja nawe unapopata fahamu baada ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Wanaweza pia kukupa dawa ya kawaida ya kutuliza maumivu, kama paracetamol.

Hadi asilimia 40% ya wagonjwa wanaweza kupata matatizo ya muda ya kumbukumbu wakati wanapopewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Kwa mfano, wanaweza kusahau mazungumzo na wageni wakati wa kipindi hiki.

Hata hivyo, kabla ya kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) takriban mgonjwa mmoja kati ya watano (17%) husema kuwa kumbukumbu zao tayari zilikuwa mbaya kiasi cha kusababisha matatizo. Ni vigumu kutofautisha athari za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwenye kumbukumbu na athari ambazo magonjwa inayotibu huwa nazo kwenye kumbukumbu.

Kwa watu wengi, matatizo ya kumbukumbu hupotea ndani ya miezi miwili ya matibabu ya mwisho na hayasababishi matatizo au huzuni.

Taratibu zote za matibabu zina hatari. Ikiwa daktari wa nusukaputi ataona kuwa si salama kukupa nusukaputi, hutaweza kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Watu ambao wamelazwa hospitalini kwa sababu ya msongo wa mawazo wana uwezekano mdogo wa kufa baada ya kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kuliko kama hawatapewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hii inaweza kuwa kwa sababu tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) huwasaidia watu kupona, au kwa sababu watu wanaopatiwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) hupokea uangalizi wa karibu wa kimatibabu.

Ni nadra sana, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kuwa inaweza kusababisha kifafa kinachodhibitiwa kinachodumu kwa kipindi cha muda mrefu. Hii itatibiwa mara moja na wafanyakazi wa afya waliopo.

Athari mbaya za kipindi cha muda mrefu

Kiwango cha athari mbaya za kipindi cha muda mrefu ni tata.

Utafiti wa kina wa kisayansi haujapata ushahidi wowote wa uharibifu halisi wa ubongo kwa wagonjwa ambao wamepewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hakuna ongezeko la hatari ya kifafa, kiharusi au ugonjwa wa akili (dementia) baada ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Athari mbaya zaidi ya kipindi cha muda mrefu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ni kwamba unaweza kusahau matukio ya zamani maishani mwako. Idadi ndogo ya wagonjwa huripoti mapengo katika kumbukumbu yao kuhusu matukio katika maisha yao yaliyotokea kabla ya kupata tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hii mara nyingi huathiri kumbukumbu za matukio yaliyojitokeza wakati, au muda mfupi kabla ya tatizo la msongo wa mawazo kuanza. Wakati mwingine kumbukumbu hizi hurudi kikamilifu au kwa sehemu, lakini wakati mwingine mapengo haya yanaweza kuwa ya kudumu. Utafiti wa hivi majuzi unapendekeza kuwa asilimia 7% ya watu wanaopokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya upande mmoja huripoti kupoteza kumbukumbu unaoendelea miezi 12 baada ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Je, ni nini kinaweza kutokea ikiwa hutapokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)?

Wewe na daktari wako mtahitaji kulinganisha hatari ya kupata athari mbaya kutokana na tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) na hatari ya wewe kutopokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Kutopokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kunaweza kumaanisha kuwa una uwezekano mkubwa wa kuwa na:

  • hali ya afya ya akili inayolemaza na ya muda mrefu
  • ugonjwa mbaya wa kimwili (na labda kifo) kwa sababu ya kutokula au kunywa
  • ongezeko la hatari ya kifo kutokana na kujiua.

Suala la kuendesha gari na tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)

Ikiwa wewe ni mgonjwa sana kiasi cha kuhitaji tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) hupaswi kuendesha gari. Shirika la DVLA linashauri kwamba hupaswi kuendesha gari wakati wa mzunguko wa kupokea matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Baada ya kumaliza mzunguko huo, inaweza kuchukua muda kidogo kabla ya kuanza kuendesha gari tena. Shirika la DVLA, kwa ushauri kutoka kwa daktari wako, litafanya uamuzi huu.

Ikiwa unapokea matibabu ya mwendelezo au udumishaji wa hali nzuri ya afya wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ili kukusaidia kuhakikisha kuwa wewe ni mwenye afya, unaweza kwa kawaida kuendelea kuendesha gari. Hata hivyo, hupaswi kuendesha gari, pikipiki au kuendesha mashine nzito kwa angalau saa 48 baada ya kila matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Uamuzi kuhusu tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)

Utoaji wa idhini ya kufanyiwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)

Kama vile matibabu yoyote muhimu katika matibabu ya dawa au upasuaji, utaombwa idhini yako, au ruhusa, ya kufanyiwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Utaelezewa matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), sababu za kuipewa na faida zinazoweza kutokea pamoja na athari zake mbaya.

Ikiwa utaamua kuendelea, utapewa fomu ya idhini ili utie sahihi. Ni rekodi inayoonyesha kuwa umeelezewa kuhusu tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), kwamba unaelewa kitakachotokea, na kwamba unatoa idhini yako ya kupewa tiba hiyo. Isipokuwa ni dharura utapewa angalau masaa 24 ya kufikiria kuhusu jambo hili na kulijadili na jamaa, marafiki au washauri wako.

Unaweza kuondoa idhini yako wakati wowote, hata kabla ya matibabu ya kwanza. Unapaswa kupewa taarifa zinazofafanua haki zako kuhusu utoaji wa idhini ya matibabu.

Taarifa zaidi kuhusu suala la kutoa idhini ya kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inapatikana kwenye(PDF).

Je, unaweza kusema matakwa yako kuhusu suala la kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) mapema?

Ikiwa una hisia kuhusu tiba ya mshtuko wa umeme (ECT), aidha unakubaliana au unakinzana, unapaswa kuarifu madaktari na wauguzi wanaokuhudumia. Unapaswa pia kuwaambia marafiki, familia au mtu mwingine yeyote ambaye ungependa akusaidie au kuzungumza kwa niaba yako. Madaktari lazima wazingatie maoni haya wanapofikiria iwapo tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inakufaa au la.

Ikiwa, wakati uko mzima, una uhakika hungetaka tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ikiwa ungekuwa mgonjwa tena, basi inafaa kuandika taarifa ya matakwa yako. Hili linaweza kujulikana kama 'uamuzi wa mapema' nchini Uingereza, Ireland Kaskazini na Wales, au 'taarifa ya mapema' nchini Scotland. Matakwa haya yanapaswa kufuatwa isipokuwa katika hali mahususi zaidi. Hii ni mada ngumu na ipo nje ya wigo wa rasilimali hii.

Baadhi ya watu ambao hapo awali wamefanikiwa kutibiwa kwa kutumia tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) wamegundua inasaidia sana hivi kwamba wamerekodi taarifa ya mapema kwamba wanataka kufanyiwa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ikiwa wataugua tena, hata kama watasema wakati huo kuwa hawataki.

Je, tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kutolewa bila ruhusa yako?

Ikiwa mtu ana 'uwezo' wa kufanya maamuzi iwapo apewe tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) au la, haiwezi kutolewa bila idhini yake iliyoarifiwa kikamilifu.

Baadhi ya watu huwa wagonjwa sana na kiasi kwamba inasemekana 'hawana uwezo' wa kufanya maamuzi kuhusu tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hii inamaanisha kuwa hawawezi kuelewa ipasavyo asili, madhumuni au athari za matibabu hayo, kukumbuka taarifa hii, au tathmini faida na hasara za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT).

Kuna sheria nchini Uingereza zinazoruhusu madaktari kufanya maamuzi kuhusu suala la kutoa matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa watu walio katika hali hii. Hizi huambatana na kinga za kisheria ili kuhakikisha matibabu yanatolewa tu ikiwa ni lazima kabisa.

Hivi ndivyo hali ilivyo kwa takriban nusu ya watu wanaopokea matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Watu ambao wanapokea tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa njia hii hupata nafuu sawa na wale ambao wameweza kutoa idhini.

Mtu anapopata afueni na 'kurejesha uwezo wa kufanya maamuzi tena' ni lazima idhini yake itafutwe tena.

Taarifa zaidi kuhusu idhini na tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) inaweza kupatikana kwenye (PDF).

Je, ubora wa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) katika hospitali yako unatathminiwa vipi?

ECT Accreditation Service (ECTAS) ni mtandao wa hiari wa huduma za afya ya akili nchini Uingereza, Wales na Ireland Kaskazini ambao unakuza mbinu bora za matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Mtandao huo husaidia kuboresha ubora wa huduma kwa kusaidia kliniki za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kutii seti ya viwango vilivyokubaliwa, kama vile masuala ya usalama na kisheria.

hufanya kazi sawa na unashughulikia kila huduma ya ECT nchini Scotland.

ECTAS na SEAN sio wadhibiti wa kisheria vya huduma za tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hili ni jukumu la Tume ya Ubora wa Huduma nchini Uingereza, Wakaguzi wa Huduma ya Afya wa Wales walioko nchini Wales, Shirika la Uboreshaji wa Huduma ya Afya la Scotland lililoko nchini Scotland na Mamlaka ya Udhibiti na Uboreshaji wa Ubora nchini Ireland Kaskazini.

Je, ninaweza kupata wapi taarifa zaidi?

Unaweza kupata taarifa zaidi kupitia viungo vilivyo hapa chini:

Kusoma zaidi

National Institute for Health and Care Excellence (NICE)

Shukrani

Taarifa hii ilitolewa na Bodi ya Wahariri ya Ushirikiano wa Umma (PEEB) ya Chuo cha Royal cha Madaktari wa magonjwa ya akili (萝莉视频). Inaonyesha ushahidi bora unaopatikana wakati wa kuandika.

Mapitio ya wataalamu na wachangiaji

  • Kamati ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) na Matibabu Yanayohusiana
  • Electroconvulsive Therapy Accreditation Service (ECTAS)
  • Scottish ECT Accreditation Network (SEAN)
  • Profesa Wendy Burn, Rais wa Zamani Aliyeachia Madaraka Hivi Karibuni na Mwenyekiti wa PEEB.

Taarifa hii ilisasishwa mnamo Machi 2022.

This translation was produced by CLEAR Global (Dec 2025)

Read more to receive further information regarding a career in psychiatry