萝莉视频

Katatonia

Catatonia

Below is a Swahili translation of our information resource on catatonia. You can also read our other Swahili translations.

Taarifa hii ni ya mtu yeyote ambaye anakumbwa na ugonjwa wa katatonia au aliyewahi kukumbwa na hali hiyo hapo awali. Pia ni ya mtu yeyote anayejua au anayemtunza mtu aliye na katatonia.

Je, katatonia ni nini?

Katatonia ni hali ambapo mtu amefungua macho lakini haonekani kujua uwepo wa watu wengine na mazingira yao. Katatonia inaweza kuathiri uwezo wa kutembea, matamshi na tabia za mtu kwa njia nyingi tofauti. Katatonia inaweza kusababishwa na mambo tofauti. Hata hivyo, sababu halisi inayosababisha mtu kuwa na hali ya katatonia sio wazi na utafiti zaidi unahitajika katika eneo hili.

Je, dalili za katatonia ni gani?

Katatonia inaweza kutokea kwa ghafla au polepole. Hapo zamani, watu wenye katatonia walisemekana kukaa katika mikao ya ajabu kwa siku nyingi mfululizo. Sasa tunajua watu walio na katatonia wanaweza pia kupata dalili zingine kadhaa.

Ikiwa mtu ana dalili tatu au zaidi kati ya hizi, anaweza kuwa na katatonia:

  • Kukaa tuli sana na kutazama angani.
  • Kukaa kwa mikao isiyo ya kawaida ambayo kwa kawaida ingeleta usumbufu.
  • Kuweka mikono au miguu yao katika mkao wowote ambao mtu mwingine anaiweka.
  • Kurudia hali moja ya kusogeza mwili kwa muda mrefu.
  • Kurudia vile mtu mwingine anafanya katika kusogeza mwili (kunakojulikana kama 'echopraxia').
  • Kurudia fungu la maneno au maneno ambayo wanasikia (inayojulikana kama 'echolalia').
  • Kufanya ishara za uso zisizo za kawaida.
  • Kukosa kuzungumza, kula au kunywa.
  • Kufanya vile wanavyoambiwa au kuelekezwa bila kuuliza swali lolote.
  • Kutofanya jambo fulani, au kupinga kufanya jambo fulani (inayojulikana kama ‘negativism’).
  • Kuwa na wasiwasi au kukosa utulivu kwa ghafla. Hali hii inaitwa 'katatonia ya kusisimka’.

Dalili hizi zinaweza kutokea na kutoweka na zinaweza kuwa mbaya zaidi au kidogo. Dalili za katatonia zinaweza kutofautiana baina ya watu. Ingawa watu wengine wanaweza kusonga kidogo tu, watu wengine wanaweza kuonekana wenye wasiwasi kabisa.

Ni muhimu kutafuta msaada ikiwa utagundua dalili hizi tatu au zaidi kwako au mtu mwingine. Msaada unapatikana kutoka kwa daktari wako wa kawaida (GP), timu ya afya ya akili au kwa kupiga simu kwa NHS 111.

Je, katatonia husababishwa na nini?

Katatonia inaweza kutokea katika hali nyingi. Hizi ni pamoja na:

Matatizo ya kiakili kama vile:

Matatizo ya kimwili kama vile:

  • maambukizi
  • jeraha la ubongo
  • matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe
  • matatizo ya kimetaboliki, k.m. ugonjwa wa kisukari – hapa ndipo  mwili hutumia kemikali muhimu kwa kiwango kingi sana au kidogo sana ambazo zinadumisha afya.
  • matatizo ya kingamwili (autoimmune disorders) – haya ni magonjwa ambayo mfumo wa kinga ya mwili, ambao kwa kawaida hupambana na maradhi, hushambulia seli zenye afya kimakosa.

Ikiwa mtu ana katatonia, timu yao ya matibabu inapaswa kuchunguza kila wakati ikiwa kuna sababu ya kimwili.

Ingawa magonjwa haya yanaweza kusababisha katatonia, njia ambayo yanafanya hivyo haijulikani.

Sio kila mtu ambaye ana matatizo haya ya kiakili na ya kimwili atapata katatonia, na hatujui kwa nini inafanyika hivyo.

Utafiti unaonyesha kwamba kemikali za ubongo kama vile GABA, glutamate na dopamine zinaweza kuhusika. Kemikali hizi huathiri jinsi ubongo unavyofanya kazi, na kuwa na kemikali hizi nyingi au kidogo inafikiriwa kuwa inahusika katika mtu kuwa na hali ya katatonia.

Katatonia pia inaweza kuathiri watu wenye matatizo ya wigo wa tawahudi (ASD). Unaweza kupata maelezo zaidi kwenye

Je, katatonia inatokea sana?

Katatonia imeripotiwa kuathiri mtu 1 kati ya 10 ambao ni wagonjwa wa kulazwa katika vituo vya afya ya akili. Hata hivyo, kuna ushahidi kwamba inaweza kuwa haijatambuliwi kikamilifu.

Mbali na kuwa na hali ya afya inayohusiana na katatonia, hatujui ni sababu gani hatarishi zinazofanya watu wengine kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata katatonia.

Kwa watu wazima, katatonia inaweza kutokea zaidi kwa wanawake kuliko kwa wanaume.

Kwa watoto na vijana balehe, katatonia haitokei kwa sana. Watoto wengi ambao wana katatonia wataipata wakiwa vijana balehe. Kwa watoto na vijana balehe, katatonia inaonekana kuathiri wavulana mara mbili zaidi kuliko wasichana.

Je, kuna vipimo gani vinavyotumika kutambua katatonia?

Kuna vipimo tofauti ambavyo daktari anaweza kufanya ili kujua ikiwa mtu ana katatonia na kile kinachoisababisha. Kujua kile kinachoweza kusababisha katatonia kunaweza kusaidia daktari kutibu katatonia.

Ikiwa inadhaniwa kuwa una katatonia, daktari wako atazingatia mambo yafuatayo:

  • Historia - Daktari atazungumza na wewe au mtu anayekutunza ili kujua kuhusu historia yako. Pia watataka kujua jinsi umekuwa ukihisi hivi majuzi. Wewe au mtu anayekutunza mnapaswa kuwajulisha kuhusu dawa yoyote unayotumia, majeraha yoyote ya kichwa ambayo huenda ulipata na matatizo mengine yoyote ya kiafya.1
  • Uchunguzi - Daktari anaweza kuchunguza tabia yako wakati wa miadi au wakati uko kwenye wadi ya hospitali.
  • Tathmini- Daktari anaweza kuchagua kukutathmini ili kuhakikisha kuwa mwili wako unafanya kazi vizuri. Huu unapaswa kuwa uchunguzi kamili wa moyo wako, mapafu, tumbo na mfumo wa neva.1,4
  • Vipimo vya damu - Daktari anaweza kufanya vipimo vya damu. Wataangalia kuona ikiwa una maambukizi yoyote au tatizo lolote la jinsi mwili wako unavyofanya kazi1,4
  • Uchanganuzi wa ubongo - Baada ya kufanya tathmini na kufanya vipimo vya damu, daktari anaweza kufanya vipimo vya picha ya ubongo ikiwa wanahitaji taarifa zaidi. Picha hii itaruhusu daktari wako kuona ubongo wako kwa kina zaidi 1,4
  • Electroencephalogram (EEG) - Kipimo hiki hufuatilia utendaji wa kielektriki katika ubongo wako1,4. Kinaweza kutumiwa kuona kama una ugonjwa wa neva. Vipimo vya Electroencephalogram hufanywa kwa kuweka sensa dogo kichwani kisha kutumia mashine kugundua ishara za kielektriki zinazozalishwa na ubongo. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu Electroencephalogram (EEG) .

Je, katatonia hutibiwaje?

Katatonia inaweza kutibiwa, na watu walio na hali hiyo wanaweza kupona kabisa. Ikiwa katatonia itagunduliwa mapema, wakati mwingine inaweza kutibiwa nyumbani. Hata hivyo, mtu aliye na katatonia mara nyingi atahitaji matibabu au msaada mkubwa zaidi. Hii inaweza kumaanisha kwamba wanahitaji kwenda hospitalini.

Kutibu tatizo msingi

Wakati mwingine, kutibu chanzo msingi cha katatonia kutatosha kutibu katatonia pia. Kwa mfano, ikiwa mtu ana ugonjwa wa wazimu, kutibu ugonjwa wa wazimu kunaweza kutibu katatonia kwa wakati mmoja. Hata hivyo, watu wengi pia watahitaji matibabu maalum ya katatonia.

Lorazepam

Katatonia mara nyingi hutibiwa kwa kutumia dawa inayoitwa lorazepam. Lorazepam ni benzodiazepine, ambayo ni aina ya dawa ya kutuliza. Hii inamaanisha kwamba husaidia kupunguza kasi ya mwili na ubongo na kulegeza misuli. Pia hutumiwa kutibu ugonjwa wa kifafa, na kwa muda mfupi inaweza kutumika kutibu wasiwasi, ukosefu wa usingizi na hofu za ghafla.

Wakati mwingine, madaktari watafikiria mtu ana katatonia lakini huenda wasiwe na uhakika. Wakati jambo hili linatokea, kabla ya kuanza matibabu kamili, daktari anaweza kumpa mtu dozi moja ya lorazepam. Hili linaitwa “challenge (jaribio)”.

Ikiwa dalili za mtu huyo zitapungua baada ya dozi moja, hii inaweza kusaidia daktari kuthibitisha utambuzi wa katatonia.

Ikiwa una katatonia, unaweza kupewa lorazepam kwa mojawapo ya njia hizi mbili:

  • Ikiwa unaweza kumeza, unaweza kumeza lorazepam kama tembe.
  • Ikiwa huwezi kumeza, unaweza kuipata kama sindano kupitia misuli au mishipa.

Mwili huvunja na kusindika lorazepam ndani ya saa chache. Kwa hiyo, mara tu katatonia inapothibitishwa na kugunduliwa, watu wengi watahitaji kutumia lorazepam zaidi ya mara moja kwa siku kwa ratiba ya kawaida. Dozi kubwa zinaweza kuhitajika kutibu katatonia kwa ufanisi.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT)

Wakati dalili za katatonia ni mbaya sana au hazipungui baada ya kutumia lorazepam, chaguo tofauti ya matibabu inaweza kuzingatiwa.

Ikiwa mtu hawezi kutembea, kula au kunywa, anaweza kuwa mgonjwa sana kimwili. Ikiwa hali hii itatokea, wanaweza kupewa tiba ya mshtuko wa umeme (ECT). Hii ni aina ya matibabu ambapo ubongo wa mtu huchochewa kwa mapigo mafupi ya kielektriki huku mtu akiwa amepumzishwa kwa kutumia nusukaputi ya jumla na akiwa amelala. Mtu anaweza kuagiziwa kozi ya matibabu ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa wiki kadhaa ili kusaidia kupunguza dalili zao.

Tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ina ufanisi mkubwa katika kutibu katatonia. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) kwa kusoma rasilimali ya tiba ya mshtuko wa umeme (ECT) ya Chuo.

Kufuatilia lishe

Wakati mtu aliye na katatonia anatibiwa, lishe yao inahitajika kufuatiliwa ili kuhakikisha kuwa ana afya nzuri. Ili kufanya hivyo, madaktari na wauguzi wanaweza kukagua vipimo vyao vya damu, mkojo na afya ya kimwili ya jumla.

Je, ni nini kitatokea ikiwa mtu hatatibiwa katatonia?

Ikiwa mtu aliye na katatonia hatapata matibabu, anaweza kuwa mgonjwa sana. Katatonia isiyotibiwa inaweza kusababisha athari zifuatazo:

  • Upungufu wa maji mwilini
  • Utapiamlo
  • vidonda vya shinikizo
  • maambukizi
  • kuganda kwa damu

Ikiwa katatonia itakosa kutibiwa, athari hizi wakati mwingine zinaweza kuua mtu.

Je watu walio na katatonia hupata nafuu?

Takriban watu 8 kati ya 10 walio na katatonia hupunguza dalili zao baada ya dozi moja ya lorazepam.

Hakuna sheria inayotumika ya muda ambayo mtu anapaswa kuendelea kutumia lorazepam, kwani watu hukabiliana vitofauti na dawa hii. Wakati mwingine mtu atahitaji dozi moja tu ya lorazepam. Hata hivyo, watu wengi watahitaji dozi zaidi ili kutibu katatonia kikamilifu.

Mara tu matibabu yanapoanza, katatonia ya watu wengi hupungua katika saa au siku chache, lakini kwa watu wengine inaweza kuchukua wiki chache.

Inafikiriwa kuwa katatonia inayosababishwa na matatizo ya hisia ina uwezekano mkubwa wa kuitikia matibabu kuliko katatonia inayosababishwa na matatizo ya kisaikolojia. Hata hivyo, matibabu ya katatonia inayosababishwa na hali zote mbili ina matokeo mazuri.

Lorazepam mara nyingi inaweza kusitishwa mara tu chanzo msingi cha katatonia kinapotibiwa. Katika hali zingine, dalili za katatonia zinaweza kurejea wakati utumiaji wa lorazepam unapositishwa. Ikiwa hili litatokea, matibabu ya kipindi cha muda mrefu zaidi yanaweza kuhitajika.

Lorazepam haipendekezwi kutumika kwa muda mrefu na inapaswa kusitishwa haraka iwezekanavyo. Wakati ikifika wa mtu kuacha kutumia lorazepam, jambo hili linapaswa kufanywa hatua kwa hatua, na lorazepam haipaswi kusitishwa ghafla.

Hata ikiwa dalili za katatonia za mtu zimepungua, bado wanaweza kuhitaji matibabu mengine kutibu chanzo msingi. Kwa mfano, ikiwa wana ugonjwa wa kimwili au hali ya afya ya akili, bado wanaweza kuhitaji matibabu kusaidia hali hizi.

Je, ninawezaje kumsaidia mtu ambaye ana katatonia?

Ikiwa unafikiri kwamba rafiki yako, mwanafamilia au mtu unayemtunza anaweza kuwa na katatonia, zungumza na daktari au muuguzi wao au wasiliana na NHS 111.

  • Kutoa taarifa - Mtu aliye na katatonia anaweza kujitahidi kutoa taarifa muhimu. Hali kadhalika, unaweza kuhitaji kujibu maswali kutoka kwa madaktari na wauguzi wao. Hii itasaidia mtu aliye na katatonia kupata utambuzi sahihi na matibabu yanayofaa.
  • Kuelezea kile kinachotokea – Watu wengine wenye katatonia wanajua kuwa wako katika hali ya kikatatonia, na jambo hili linaweza kuwa la kuchanganya na la kutisha kwao. Unaweza kuwasaidia kwa kuwaelezea kile kinachotokea.
  • Kuelezea kile kilichotokea - Watu wengine wenye katatonia hawawezi kukumbuka jinsi walivyohisi wakati walikuwa katika hali ya kikatatonia. Wakati mtu unayemjua hayuko tena katika hali ya kikatatonia, anaweza kuona ni jambo la manufaa na la kutuliza ukimweleza kilichotokea.
  • Kutembelea - Ikiwa unatembelea mtu aliye na katatonia, jaribu kuwa mtulivu. Watu walio na katatonia mara nyingi wanaweza kusikia watu walio karibu nao wakizungumza, hata kama wao wenyewe hawaongei, kwa hiyo inaweza kusaidia kuzungumza na mtu unayemtembelea.
  • Kula - Ikiwa mtu aliye na katatonia hali, jaribu kumletea chakula ambacho unajua anapenda na kukifurahia.

La kusoma zaidi

Ikiwa una katatonia, daktari au muuguzi wako atajibu maswali yoyote unayoweza kuwa nayo na anaweza kukupa maelezo zaidi.

Unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu katatonia hapa:

  • - ukurasa huu wa wavuti una taarifa kuhusu katatonia kwa madaktari, wagonjwa na watunzaji.
  • – taarifa hii inaangazia jinsi katatonia inaweza kuathiri watu walio na tawahudi. Inajumuisha miongozo kwa watu wazima wenye tawahudi, wazazi na watunzaji, na wataalamu.

Heshima kwa

Taarifa hii ilitolewa na Bodi ya Wahariri ya Ushirikiano wa Umma (PEEB) ya Chuo cha Royal cha Madaktari wa Magonjwa ya Akili (萝莉视频’ Public Engagement Editorial Board). Inaonyesha ushahidi bora unaopatikana wakati wa kuiandika.

Waandishi wa kitaalam: Dkt Emma Salter, Dkt Husam Khalil, Dkt Nabeel Helal

Marejeleo kamili ya rasilimali hii yanapatikana inapoombwa.

This translation was produced by CLEAR Global (Dec 2025)
Read more to receive further information regarding a career in psychiatry